Wazazi, walezi chukueni tahadhari mnapowavalisha watoto nguo
Mara nyingi wazazi na walezi walio na watoto wadogo hasa wale wachanga wa chini ya miezi sita, ndiyo wanaokuwa na mashaka zaidi na joto la mwili linapokuwa juu baada ya kuhisi kwa kumgusa. Lakini mara nyingine njia ya kumgusa mtoto haiwezi pekee kukusaidia kujua mtoto huyo ana homa.
Kipimajoto kama kinavyojulikana kitabibu kwa jina la ‘Thermometer’ ndiyo kifaa sahihi cha kupima joto. Bei ya kifaa hiki kinaanzia Sh5,000 hadi Sh10,000.
Niwakumbushe, ni vizuri kuwa nacho nyumbani.
Lakini wazazi wanakosa ufahamu wa kuweza kujua kuwa hili ni joto la kawaida na hili ni la homa.
Kwanini kupanda kwa joto la mwili?
Kupanda kwa joto la mwili wa binadamu ni matokeo ya mambo mengi, miongoni ni pamoja na kuvamiwa na vimelea wa maradhi.
Joto la mwili kuwa juu kwa mtoto mwenye chini ya mwezi mmoja au mwenye wiki moja, ni jambo ambalo mzazi au mlezi hapaswi kulipuuzia.
Mzazi kujua njia ya kuweza kujua joto la mtoto kuwa ni homa au ni joto la kawaida ni muhimu, hiyo inasaidia kukupatia tahadhari na ukawahi hospitali mapema.
Kutokana na kukuwa kwa sayansi, hivi sasa vipimajoto vinapatikana kwenye maduka mengi yanayouza dawa za binadamu kikiwa katika mfumo wa Kielektroniki.
Unatakiwa kukiweka kwenye kwapa la mtoto na ukibane vema kwa dakika moja, kitakupatia majibu ya joto la mtoto.
Kwa kawaida, joto la binadamu ni nyuzijoto 37 au 36.9,
lakini wataalamu wa afya wameweka mpaka. Endapo joto hilo litazidi nyuzijoto 37.5 na kuendelea, huhesabika hiyo ni homa. Linapovuka kuanzia 38.5 na kuendelea hiyo ni ishara ya mtu kuwa na homa kali, ikifikia nyuzijoto 39, hapo ndipo huanishwa kuwa ni dalili ya hatari na huenda ikawa ana ugonjwa mkali mwilini.
Wanasayansi watafiti duniani wanaamini kupanda kwa joto la mwili ni moja ya njia ya mwili kujihami na kupambana na vimelea wa maradhi ya virusi, bakteria, fangasi, sumu za vimelea na vitu vingine vilivyoingia ndani ya mwili. Inaaminika kupanda kwa joto la mwili kunawafanya vimelea wa maradhi waliovamia mwilini kupata wakati mgumu, sababu mazingira hayo si mazuri kwao.
Mwili wa mwanadamu ni mashine yenye mambo mengi. Miongoni ni mfumo maalumu unaodhibiti joto la mwili. Vimeng’enya na homoni ni vitu vya mwili vinavyohitaji jotoridi la wastani kuweza kufanya shughuli za mwili.
Je! Homa hutokana na nini
Homa hutokea wakati mazingira ya ndani ya mwili yanapopandisha joto na kupita kile kiwango cha kawaida. Kituo kikuu cha udhibiti wa joto la mwili kipo kwenye sehemu ya ubongo inayoitwa ‘Hypothalamus.’ Kituo hicho ndicho kinafahamu joto la mwili linapaswa kuwa nyuzijoto 37 na hutuma ujumbe mwilini kuhakikisha kiwango hicho kinabaki hivyo hivyo.
Kwa kawaida, joto la mwadamu hubadilika kidogo mchana lakini asubuhi linakuwa chini na jioni huongezeka kidogo kulingana na mazingira hasa ya watoto ambao hucheza na kufanya mazoezi.
Kwanini joto la mtoto hupanda?
Joto la mwili wa mtoto linaweza kupanda na kuwa homa kutokana na sababu mbalimbali. Miongoni ni upungufu wa maji mwilini, kuvalishwa au kufunikwa na nguo nyingi akiwa katika mazingira ya joto kali.
Ikimbukwe kuwa mwili wa mtoto mchanga hauna uwezo wa kuhifadhi joto, ni vizuri kumvalisha mavazi yenye kutunza joto lakini ukiwa mwangalifu asipoteze wala kuliongeza sana.
Njia nzuri ni kujitazama mzazi au mlezi hapo ulipo umevaa nguo ngapi zinazokufanya upate utulivu, yaani kuhisi joto ni la kawaida, kama una safu moja ya nguo mwilini mwako, basi mtoto mvalishe mbili. Sababu nyingine ambayo ina uzito mkubwa kusababisha homa ni uambukizi wa vimelea vya maradhi wakiwamo bakteria na virusi.
Mwili unapovamiwa na vimelea, mfumo wa kinga ya mwili hujibu mapigo baada ya kupewa taarifa na ubongo. Mwili hutiririsha askari mwili pamoja na kemikali mbalimbali ikiwamo ya ‘prostaglandin’ ambayo husababisha joto la mwili kupanda. Kupanda kwa joto kunaweza kuwa na faida mwilini mwa mtoto ikiwamo ya kuwanyima mazingira rafiki virusi ambao kiasili hawapatani na joto la juu, jambo hili linatoa nafasi kwa kinga ya mwili kuviharibu kirahisi. Kwa ujumla mwili hunufaika na homa kwa kuweza kupambana na uvamizi wa vimelea vya maradhi.
Ingawa mara nyingine homa inapokuwa kali sana huweza kuchangia kujitokeza kwa dege dege.
Watoto wachanga wa chini ya miezi mitatu wana kawaida ya wakuzaliwa na kinga ambayo ni changa kuweza kupambana na maradhi. Endapo utamgundua ana homa, haraka unatakiwa kumrudisha hospitalini kwani huenda ikawa ni ishara ya uambukizi wa kitovu ambao ni hatari kwa maisha ya mtoto.
Ni makosa makubwa yanayofanywa na wazazi wengi kujichukulia uamuzi wakumpatia dawa kiholela ya kutuliza homa hasa paracetamol ya vidonge au ya maji. Kufanya hivi kwa watoto wa chini ya miezi miwili au siku 40 sio sahihi, dawa hii haipaswi kutumiwa na watoto hao kwakuwa ini lao bado changa halina uwezo wakustahimili makali yake inapoivunja vunja.
Dawa nyingi hufika katika ini kwa ajili ya kuvunjwa vunjwa na kuendelea na hatua zingine mpaka kutolewa nje ya mwili kwa njia ya figo, haja kubwa na jasho. Watoto wachanga wa chini ya miezi miwili homa zao hutokana na maambukizi ya bakteria wanaogusana na mwili wake anapozaliwa au kupata uambukizi wa kitovu.
Joto la mtoto mchanga linashushwaje?
Ili kushusha joto la mtoto mchanga unatakiwa kumpunguzia nguo alizovaa na kumwacha wazi kwanza mpaka litakaposhuka. Kwa upande wa tiba, anatakiwa apatiwe antibayotiki za mshipa au za kunywa ili kuangamiza vimelea waliochokoza mwili kupandisha joto.
Njia salama ya kumsaidia kushusha homa ni kumkanda na maji ya kawaida au pamba na spiriti mwili.
Haishauriwi kumkanda na maji ya baridi yaliyokuwa kwenye jokofu kwani hushusha joto ghafla na kwa kufanya hivyo inaweza kusababisha kifo.
Ukiacha sababu za joto kupanda kwa kuvalishwa nguo nyingi, kumbuka homa ni kiashiria kwa mwili kuvamiwa na vimelea au kuumwa na ugonjwa flani.
Unapoona homa hiyo imeambatana na dalili zingine kama za degedege, kupoteza fahamu, kulegea sana, kushindwa kunyonya, kutapika kila kitu anachokula na kupumua kwa shida, ni vizuri kuwahi hospitali au katika kituo cha afya na zahanati kupata huduma zaidi za matibabu. Epuka kumpatia mtoto dawa za kutuliza homa bila kushauriwa na daktari, kwakuwa joto linapopambana haimaanishi ni homa. Ripoti tatizo......
Usisahau ku follow page yetu kwaajili ya elimu mbalimbali
Comments
Post a Comment
+255769571079